Mpya
Taji la ubaya 46-50
TAJI LA UBAYA
(A crown of badness)
Mtunzi: "Mwaki Ze Done"
Sehemu 46.
"Dear nimekuletea zawadi, najua utaipenda" yaani shaifa alikuwa anaongea sauti tamu ambayo hata wewe mpenzi msomaji ungesikia, hata bila kumuona ungempigia kura ya Umiss dunia.
Jacob alibaki anakenua meno tu kwa furaha maana aliletewa matunda aina ya apple na siku hiyo Jacob aliona matunda matamu kama ndo hajawahi kula vile,(kweli chakupewa na mpenzi kinanoga)
Fatuma Naye alipewa matunda na Shaifa ila kwake ilikuwa tofauti yeye aliona yale maapple machungu kama ndimu maana alikuwa anaumia jinsi anavyo ona Jacob na shaifa wanashikana.
Zilipita siku tatu, yaani mapenzi ya Jacob na shaifa yalikuwa yamekolea ni hatari, ilifika kipindi mpaka Jacob akawa anasahau kama mule ndani kuna mtu anaitwa Fatuma.
Kutokana na maumivu ambayo fatuma alikuwa anayapata Jacob akiwa na Shaifa aliamua kuhama pale nyumbani na kurudi kwenye zile nyumba za Mr jomo walizo kuwa wanakaa mwanzo na hakuogopa kwamba atakamatwa na akina Mr Derick maana uvumilivu ulikuwa umemshinda.
Maisha yaliendelea ilipita miezi miwili, Jacob akiwa amemusahau Fatuma kabisa na swala la matumizi kwa Fatuma halikuwepo kabisa, kipindi hicho shaifa tayari alikuwa na ujauzito wa mwezi mmoja, wakati upande wa pili kwa Fatuma Naye tayari alikuwa ana ujauzito wa kama miezi miwili na Fatuma tayari alikuwa amemaliza chuo na kipindi hicho alikuwa anasubiri kazi tu.
Kutokana na ugumu wa maisha Fatuma siku moja aliamua kumpigia simu Jacob walau amuombe hata pesa ya matumizi kidogo maana alikuwa hana pesa ya kula kabisa.
Fatuma alipiga simu kama Mara kumi hivi simu ilikuwa haipokelewi, mwishowe iliacha kupatikana kabisa.
Fatuma hakukata tamaa jioni alipiga tena kama mara tano hivi mara ya sita ilipokelewa na aliye pokea alikuwa ni Shaifa
"Helloo Fatuma wasemaje??" Ilikuwa ni sauti ya Shaifa
"Dada shaifa shikamo" yaani maisha ww yasikie tu, Fatuma aliamukia kwa heshima siku hiyo na alibaki mdomo kama pilitoni
"Marhaba mtoto mzuri eheee wasemaje sasa? " Shaifa aliitika kwa Madaha kabisa
"Samahani naomba kuongea na Jacob" Fatuma aliongea
"Fatuma we nambie tu kwani unataka kuzungumza kipi hasa cha siri na mume wangu??" Shaifa alikuwa na Wivu siyo wa nchi hii.
"Dada shaifa mi nataka niombe pesa kidogo ya matumizi" Fatuma aliongea kinyonge
"Fatuma bana kwa hiyo hilo ndo ulikuwa unaogopa kunambia?? Basi poa Jacob yupo hapa ila anaangalia mpira na kasema hataki usumbufu, ila usijali mwaya unatumiwa pesa baadae kidogo" Shaifa aliongea na kukata simu.
Walau Fatuma alitabasamu kidogo maana alijua anaenda kupata pesa.
Siku hiyo Fatuma alisubiri pesa itumwe mpaka alichoka, yaani ilifika saa nne usiku pesa bado haijatumwa na Fatuma Naye alikuwa anahitaji kula, akichoka kusubiri mpaka usingizi ukawa umempitia.
Fatuma alikuja kushituka asubuhi kusha kucha, alichukua simu yake walau aangalie kama katumiwa pesa ila hakuona kitu.
Aliamua kumpigia simu Jacob tena ili amkumbushe, aligundua kwamba namba yake imeblokiwa maana simu ilikuwa inakataa bila hata kuita.
Fatuma siku hiyo alilia mpaka alichoka, alikumbuka jinsi walivyo pambana na Jacob kurudisha zile mali, alibaki anaangalia tu na kila kitu alimwachia Mungu.
Fatuma alipata akili mpya, ilibidi aamuke na kwenda kwenye kampuni ya Jacob mojawapo na alipo fika kule kwa kuwa alikuwa anajulikana kama mke wa Jacob aliamua kudanganya kwamba kuna pesa amekuja kuchukua katumwa na Jacob.
Kwa kuwa manager alikuwa anamjua Fatuma vizuri na ni mara nyingi alikuwa anakuja hapo kuchukua pesa basi, ilibidi amwamini na kumpa pesa kiasi cha Tshs milioni 10.
Baada ya Fatuma kupewa pesa hizo aliamua kuhamia mkoa mwingine kabisa maana aliona kuendelea kukaa pale anaweza jiletea matatizo na ukizingatia yeye ni mjamzito alafu sekeseke la Mr Derick bado halijaisha.
Jacob na Shaifa mambo yalikuwa motomoto, na Jacob alikuwa ashamzoea shaifa tayari na vile vimbwanga vyake.
Jacob kuna siku alienda kutembelea moja ya kampuni zake, baada ya kufika huko alipewa taarifa kwamba mkewe Fatuma alikuja kama wiki moja iliyopita kuchukua pesa na alidai ametumwa.
Jacob alipo pewa taarifa hizo alikasirika mno na aliamua kukanyaga mafuta mpaka kwenye ile nyumba ya Mr jomo ambako yeye alijua bado Fatuma yupo huko.
Alipo fika alishanga kuto ona mtu na vitu vyote vilikuwa vimehamishwa mule ndani
"Kudadeki huyu mpuuzi atakuwa kahamia wapi sasa?" Jacob alijiuliza ila hakupata jibu aliamua kurudi nyumbani akiwa kakasirika kweli kweli, Jacob alipo fika nyumbani kwake kabla hajaingia alishangaa kuona kama nyumba yake inafuka moshi kwa ndani, hapo Jacob hofu ilimjaa zaidi.
Alipo ingia ndani hakuamini macho yake, aliona kundi la wanawake wakiwa uchi walikuwa wamemzingira mke wake shaifa hapo Jacob hofu ilimuingia
"Nyie ni kina nani??" Jacob aliongea kwa hofu na uoga mkubwa mno.
Wale wanawake walimgeukia Jacob na wote walikuwa wameshika vitana vya kuchania nywele na vitana hivyo vilikuwa vinatoa moshi ambao ndo ulikuwa umesambaa nyumba nzima.
"Miss shaifa chagua moja huyu mume wako auawe au ufe wewe?? Mama mmoja aliyekuwa na jino moja tu mdomoni mwake Aliongea na alionekana yeye ndo kiongozi wa kundi hilo.
Itaendelea......
Usikose sehemu ya 47.
TAJI LA UBAYA
(A crown of badness)
Mtunzi: "Mwaki Ze Done"
Sehemu 47.
"Miss shaifa chagua moja huyu mume wako auawe au ufe wewe?? Mama mmoja aliyekuwa na jino moja tu mdomoni mwake Aliongea na alionekana yeye ndo kiongozi wa kundi hilo.
Jacob bado alikuwa haelewi ni mchezo gani unaendelea mpaka hapo.
"Jacob mi nakufa nikiwa bado nakupenda, naomba nikifa jaribu kumtafuta mdogo wangu Sharifa ukae naye, pia naomba usimuache Fatuma kwa kuwa anakupenda mno" Shaifa aliongea Maneno ambayo yalimfanya Jacob atoe machozi maana yale yalikuwa maneno machungu mno kwa Jacob.
"Shaifa hatutaki ngonjera chagua moja, maana umetusumbua kwa muda mrefu kwa hiyo hatupendi usumbufu zaidi?" Yule mama aliongea tena kwa sauti ya mkazo
"Niuweni mimi, mume wangu muacheni" Shaifa aliona bora yeye ndo afe.
Wale wanawake hawakutaka tena mjadala kwa kuwa alikuwa kachagua mwenyewe hawakutaka kuchelewa, walichukua Kitana mojawapo na kuanza kumvukisha ule moshi Shaifa puani, shaifa hakuchukua hata dakika tano, tayari alikuwa amekata moto.
Baada ya hilo tukio wale wanawake walipotea kimiujiza, Jacob alibaki pale na maiti ya Shaifa, Siku hiyo Jacob alilia kilio ambacho hakina mfano.
Baada ya kifo cha Shaifa taarifa zilisambaa kwa majirani, ndugu na jamaa wa Jacob kwakuwa wengi walikuwa washaanza kumfahamu shaifa.
Baada ya hapo maandalizi ya mazishi yalifanyika hatimaye Shaifa alizikwa, Jacob alilia sana ila ndo hivyo ilikuwa haisaidii kwa sababu yaliyo tokea ndo yashatokea.
Jacob hapo alianza kuishi maisha ya upweke, maana jumba kubwa lakini alikuwa anakaa pekee yake, hapo Jacob alianza kuona maisha magumu angali pesa anayo, alikuwa anatamani kutafuta mwanamke mwingine lakini ndo hivyo zile mila za akina Fatuma zilikuwa zinamfunga maana kila mwanamke ambaye ni binadamu wa kawaida akilala naye tu, alikuwa anafariki.
Upande wa akina Mr Derick baada ya kugundua Shaifa ambaye wao ndo walikuwa wanamuogopa kipindi chote kafa, hapo walifurahi sana waliona kazi yao inaenda kutendeka tena kiwepesi kabisa, maana kipindi chote hicho walikuwa wamesitisha mpango wao baada ya kugundua Shaifa siyo binadamu wa kawaida na shaifa alikuwa habanduki kwa Jacob kwa hiyo walishindwa namna ya kutekeleza mpango wao ila baada ya Shaifa kufa tu hapo mpango wao ulifufuka upya tena kwa kasi.
Jacob yeye alikuwa ashasahau kabisa kwamba kuna mtu anaitwaga Mr Derick anamuwinda, na Jacob alikuwa anaendelea na kazi zake kama kawaida maana tayari maisha ya upweke alikuwa ashaanza kuyazoea.
Siku moja Jacob akiwa anatoka nyumbani kwake asubuhi, alimuona Ediga mitaa ya pale kwake akiwa anazunguka zunguka na Camera, hapo Jacob alikumbuka kwamba bado hajamalizanaga na akina Mr Derick na hapo Jacob aligundua yupo kwenye danger.
Jacob baada ya kumuona Ediga alizuga kama ndo hajamuona vile, alirudi ndani na kuchukua nyaraka zote na pesa, kisha alifunga milango vizuri na kuondoka, Jacob alipanda gari na kuondoka, ila anavyo ondoka aliona kwa nyuma kuna pikipiki inamfuatilia.
Jacob moyo ulikuwa unadundia chini ya matako jinsi ambavyo alikuwa anaogopa, maana alijua awamu hii akizembea anakufa maana mtu wa kumsaidia hayupo tena.
Jacob hapo alizuga kama ndo anaenda kwenye ile nyumba yake nyingine ambayo ndo Vicky alikuwa anakaa mara ya kwanza na hiyo nyumba ilikuwa haikaliwi na mtu yeyote maana alikuwa bado hajaipangisha.
Jacob alifika kwenye nyumba hiyo alifungua geti na kuingiza gari ndani alipo angali aliona yule mwenye pikipiki kule nyuma ni kama anapiga simu kutoa maelekezo kwa mtu.
Jacob baada ya kuingiza gari mule ndani, alilipaki na kuiingia ndani kabisa, nyumba hiyo ilikuwa na mlango wa Nyuma ambao ulikuwa ni wa siri, yaan mlango huo pamoja na Vicky kukaa muda wote hapo alikuwa hajawahi kujua kama kuna mlango wa nyuma.
Baada ya Jacob kuingia ndani, alipitia mlango wa nyuma na kutoka, na mkononi alikuwa ameshika begi lenye nyaraka zote.
Baada ya kufika barabarani aliita tax na kupanda, alitoa maelezo sehemu ya kumpeleka.
Ilipo fika usiku tu mida ya saa mbili, tayari Mr Derick na kikosi chake walikuwa wametimba kwenye nyumba hiyo ambayo ndo Vicky alikuwa anakaa wakiwa wanatarajia kwamba Jacob yumo ndani, na walipo ona gari bado limepaki pale getini hapo ndo walipata uhakika kwamba Jacob yupo ndani, yaan Mr Derick alikuwa anakenua meno kwa furaha.
Waliingia mule ndani wakiwa makini kweli ili mwali wao asije kimbia maana walijua ni uhakika kwamba Jacob yumo.
Itaendelea......
Usikose sehemu ya 48.
TAJI LA UBAYA
(A crown of badness)
Mtunzi: "Mwaki Ze Done"
Sehemu 48.
Waliingia mule ndani wakiwa makini kweli ili mwali wao asije kimbia maana walijua ni uhakika kwamba Jacob yumo.
Jacob naye huku kwenye taxi, alielekeza kwamba apelekwe porini mpaka huyo mwenye taxi mwenyewe alishangaa, maana baada ya kufika porini sehemu ambayo Jacob alidai wamuache ilikuwa ya kutisha.
Jacob akiwa kashika lile box la nyaraka alianza kuzama ndani ya pori kabisa na alikuwa hata haogopi kitu chochote.
Baada ya Jacob kutembea kama nusu saa kule porini alitafuta sehemu nzuri na kuanza kuichimba, alikuwa anatumia Miti mikavu iliyo chongoka vizuri kuchimba maana ardhi yenyewe ilikuwa siyo ngumu.
Baada ya kuchimba na shimo kuwa refu kidgo Jacob alifukia lile box, na aliweka alama maeneo hayo, baada ya kazi hiyo Jacob alianza kurudi barabarani ili apate usafiri wa kumrudisha mjini japo ilikuwa ni usiku ila aliamini kwamba atapata usafiri.
Huku kwa akina Mr Derick baada ya kuingia mule ndani walianza kutafuta, walitafuta Zaid ya masaa manne ila bado hawakuona kitu
"Hivi Ediga una uhakika mulimuona kabisa anaingia humu ndani na gari" Derick alianza kupata wasi wasi
"Boss ni uhakika alikuwa yeye kwa sababu sisi tulimfuatilia toka anatoka nyumbani kwake mpaka huku na hizi ni baadhi ya picha ambazo nilimpiga akiwa anatoka" Ediga alikuwa anamthibitishia Mr Derick kwamba ni Jacob waliye muona wala siyo mwingine.
"Duuu!! Basi hii nyumba itakuwa ina chumba cha siri, kama sivyo basi ina mlango mwingine wa kutokea" Mr Derick alianza kupata wasi wasi
Walianza upya kutafuta walitafuta mpaka saa tisa usiku hawakuona kitu chochote, hapo ilibidi warudi majumbani kwao maana walishindwa kupata kile walicho kuwa wanakihitaji.
Jacob naye alifanikiwa kurudi mjini na alifikia kwenye hoteli maarufu pale mjini, alilala mpaka asubuhi, Jacob baada ya kuamuka alianza kufikiria namna ya kupambana na Mr Derick, Jacob aliwaza ila aliona kama kila anacho kiwaza kitamkamatisha hapo ilibidi atulize kichwa kwanza.
Akina Mr Derick hawakukoma kumtafuta Jacob, ilipita miezi kama sita hivi Jacob akiwa bado anawakwepa akina Mr Derick yaani alikuwa anaishi kama ndege japo pesa alikuwa nayo (hapo ndo utaamini pesa siyo kila kitu), na Jacob alikuwa ameshamiss uwepo wa Fatuma ila ndo hakujua atampata wapi alijaribu kumtafuta Fatuma ila alishindwa kujua wapi alipo.
Siku moja Jacob katika pitapita yake mjini alikutana uso kwa uso na Mr Derick, bahati nzuri kwa Jacob Mr Derick siku hiyo hakuwa na wapambe wake alafu ilikuwa ni katikati ya watu kwa hiyo asingeweza kufanya kitu chochote, ila walipishana kama hawajuani na Mr Derick alimpiga jicho kali mno Jacob, mpaka Jacob alishituka.
Jacob kwa kuwa alikuwa na gari, hakutaka kuchelewa maeneo hayo maana aliona akizidi kuzurura anaweza kamatwa, ila Jacob anavyo ondoa gari tu pale sokoni aligundua kuna gari inamfuatilia nyuma, Jacob alicho kifanya alisimamisha gari ili aone yule wa nyuma atafanyaje.
Jacob aliliona lile gari la nyuma linazidi kusogea na lilipo karibia kufika pale alipo paki Jacob nalo lilipaki, ila Jacob alipo angali kwenye site mirror yake aligundua ni Mr Derick.
Upande wa Fatuma akiwa mkoani tayari alikuwa ashajifungu mtoto wa kiume na mtoto huyo alimwita jina la Deus yaani jina la baba yake na Jacob.
Fatuma alikuwa anaishia maisha ya kawaida sana maana alikuwa ashafungua duka la matumizi ya nyumbani na hilo ndo lilikuwa linamsaidia yeye kuendesha maisha yake ya kila siki.
Fatuma akiwa kule mkoani alitumiwa taarifa za kwamba amepata kazi katika hospitali ya rufaa maana yeye alikuwa amesomea udakitari, baada ya taarifa hizo Fatuma alifurahi mno maana aliona maisha yake yanaenda kuwa angalau mazuri na alikuwa anahitajika kwenda kuripoti ndani ya mwezi huohuo.
"Yes narudi tena mjini, yawezekana nikamuona na Jacob Wangu jamani maana ni kitambo, na sijui wanaishi salama na shaifa!!?" Fatuma baada ya zile taarifa alikuwa anajisemea mwenyewe kwa furaha, pamoja na mateso yote yale aliyo yapitia Fatuma kwa Jacob ila bado mtoto wa kike alikuwa hajamsahau Jacob na alikuwa kammiss ni hatari na alikuwa hajui kama shaifa ashatangulia mbele za haki.
Huku kwa Jacob, baada ya kusimamisha lile gari aliona na gari la nyuma limesimama, Jacob ilibidi atulie ili aone Mr Derick anataka kufanya nini, ila Jacob kupita kioo chake alimuona Mr Derick kwa nyuma ndani ya gari lake ni kama anashikashika bastola yake.
Itaendelea......
Usikose sehemu ya 49.
TAJI LA UBAYA
(A crown of badness)
Mtunzi: "Mwaki Ze Done"
Sehemu 49.
Huku kwa Jacob, baada ya kusimamisha lile gari aliona na gari la nyuma limesimama, Jacob ilibidi atulie ili aone Mr Derick anataka kufanya nini, ila Jacob kupita kioo chake alimuona Mr Derick kwa nyuma ndani ya gari lake ni kama anashikashika bastola yake.
Hapo Jacob hakutaka kusubiri aliondoa gari kwa speed Kali mno mpaka Derick mwenyewe alishituka, Derick alijitahidi kufuatilia ni njia gani Jacob kaingia ila hakuona.
Jacob alienda moja kwa moja mpaka hotelini, alitulia na kuanza kutafakari hapo aliona akizembea sana Jacob atamuzoea, aliona ni bora iwe jino kwa jino.
Alicho kifanya Jacob alitafuta wale vijana wahuni wa kitaa walio choka na maisha yaani wenyewe kufa wanaona poa tu, Jacob aliwatafuta kama watano aliwaelekeza mchongo ambao yeye anataka kudili nao, kutokana na pesa ambazo aliwaahidi, wale jamaa hata hawakutaka kudiscuss sana.
Kitu alichokuwa amekipanga Jacob kilikuwa ni kwanza kumfirisi Mr Derick ili asiwe na nguvu ya kumsumbua, basi aliapanga kwenda kurihalibu duka lake la vipodozi ambalo Derick alikuwa kalifungua huko uswahilini anako kaaa na lilikuwa ni duka maarufu huko uswahilini na ndilo lilikuwa duka kubwa kuliko maduka yote ya huko, na hilo duka Mr Derick alikuwa analitegemea kwa asilimia 60 .
Vitega uchumi vikubwa vya Mr Derick ilikuwa ni hilo Duka, gereji mbili alizokuwa kafungua, pamoja na kipub alichokuwa amefungua huko uswahilini hivyo ndivyo vilivyo kuwa vinamuweka Mr Derick mjini kwa kipindi hicho na lengo la Derick ilikuwa ni kurudi katika maisha ya kibilionea aliyo kuwa anaishi na ndo maana alikuwa anamfuatilia sana Jacob.
Jacob na wale vijana alio watafuta walipanga mipango yote kama inavyotakiwa na kilicho kuwa kimebakia ilikuwa ni kutekeleza tu.
Upande wa Vicky huku, mambo yalikuwa yameanza kuharibika maana mzee aliyekuwa anamuweka mjini na kumfadhili alikamatwa baada ya kukutwa na madawa ya kulevya, kwa hiyo Vicky alikuwa hana nyuma wale mbele na kibaya kwake Chuo aliishia njiani, huwenda angemalizia angebahatika kupata kazi ambayo ingemshikia mdhamana.
Vicky ilibidi apange chumba, na pesa ya kulipia alikuwa anaipata kwa mazingira magumu kweli, bahati mbaya kwa Vicky mitaa yote alikuwa anajulikana kama mtu wa kutembea na vibabu kwa hiyo wengi walio kuwa wana mtongoza Vicky walikuwa ni wazee, vijana wa umri wake walikuwa wanamkwepa na Vicky naye alikuwa amechoka maisha ya kutembea na wazee alikuwa anataka apate mwanaume wa size yake wapendane kwa dhati na wafunge ndoa.
Hapo Vicky ndo alianza kuelewa maana ya maisha, maana kwa kipindi hicho kitu alicho kuwa anakitaka alikuwa hakipati bali vilikuwa vinajitokeza ambavyo yeye havitaki.
Huku upande wa akina Jacob Ilikuwa ni usiku wa manane, Jacob na wale vijana alio watafuta walionekana wanakatiza mitaa ya uswahilini na kilicho tokea usiku huo sisi hatukuwepo ila malaika wetu walikuwepo.
Mr Derick akiwa amelala mida ya alfajiri kama saa kumi na moja hivi alisikia simu inaita, wakati hiyo ilikuwa siyo kawaida, baada ya kupokea simu hiyo alipokea taarifa ambazo zilimfany ashituke na kutumbua macho pale kitandani.
"Dear kulikoni mbona unashituka hivyo??" ilibid mke wake amuulize baada ya kuona jamaa kashituka nusura ya kuangusha simu.
"Heeee heeee!! We mwanamke hivi unavyo funga kule dukani jioni uliacha kupo sawa kabisa??" Mr Derick akiwa anavaa suruali kwa haraka alimuuliza mke wake
"Jamani mbona nilifunga vizuri kabisa na niliacha usalama wa kutosha kwani vipi??" Naye Mama Jacob ilibidi aamuke huku akiwa bado haelewi nini shida.
" Bwana wew kuna mtu kanipigia simu saaa hii eti duka letu la vipodozi linaungua huko barabarani" Mr Derick anavyo ongea tayari muda huo alikuwa amefika mlangoni ili atoke kwenda kushuhudia.
Derick alifika pale alipo paki gari analotembeleaga, jamaa alipanda gari bila hata kuangalia kama gari ipo vizuri ama laa yeye alipanda tu, Mr Derick alijaribu kuwasha gari ila lilikuwa haliwaki, alipo shuka kuangalia alikuta kila kitu kwenye gari kipo ovyo!! Kwanza kwenye injini ya gari ilikuwa imejazwa chumvi ya kutosha, pili betri ya gari ilikuwa imechomolewa na matairi ya gari yalikuwa yametobolewa ovyoovyo.
Baada ya Mr Derick kugundua hilo kijasho chembamba kilianza kumtoka yaani alikuwa kachanginyikiwa ilibakia kuvua nguo tu.
Mke wake alitoka ndani akiwa anafunga vibwebwe ili naye akajishuhudie huko wanako sema duka limeungua ila alipo fika nje alikuta mme wake anajikanyaga ovyoovyo, mara ashike kichwa mara ashike matako, mara pua, mara atie mikono mfukoni yaani ilikuwa ni kizaazaa.
"Heee!! We mwanaume vipi ndo kuchanganyikiwa ama mi nikajua utakuwa umefika eneo la tukio kumbe upo hapa unarandaranda tuu?" Mama Jacob alishangaa kumuona Mr Derick bado yupo pale nje anazunguka tu.
Baada ya maneno hayo Mr Derick ni kama ndo alishitushwa, hapo alianza kukimbia kwa miguu kukata mitaa, alipita vichochoro na vichochoro mpaka kufika eneo la tukio, naye mke wake alikuwa anafwata nyuma.
Baada ya kufika pale eneo la tukio Mr Derick na Mama Jacob walibakia wameshika vichwa maana duka ndo lilikuwa linaishia kuungua na walikuta nyomi ya watu wakiwa wanashangaa, yaani Mr Derick alikuwa anapewa pole ila yeye aliona kama anatukanwa tuu, maana katika miradi yake aliyokuwa anategemea kwa asilimia kubwa ni hilo duka la vipodozi na mapambo.
Mama Jacob tayari alikuwa ashazimia baada ya kuona lile tukio maana yeye ndo alikuwa anasimamia hilo duka, yaani alikuwa anauza na alikuwa ameajiri mabinti kama watatu hivi ambao alikuwa anasaidiana nao kuuza.
Watu walikuwa wanampepea Mama Jacob, Yaani hapo Mr Derick ndo alizidi kuchanganyikiwa kabisa, huwezi amini na ubabe wote wa Mr Derick siku hiyo alilia kama mtoto kanyimwa pipi.
Itaendelea......
Usikose sehemu ya 50.
TAJI LA UBAYA
(A crown of badness)
Mtunzi: "Mwaki Ze Done"
Sehemu 50.
Watu walikuwa wanampepea Mama Jacob, Yaani hapo Mr Derick ndo alizidi kuchanganyikiwa kabisa, huwezi amini na ubabe wote wa Mr Derick siku hiyo alilia kama mtoto kanyimwa pipi.
Baada ya kuona Mama Jacob hazinduki anazidi kupoa tu ilibidi ufanyike mpango wa kupelekwa hospitalini kwa ajili ya huduma zaidi.
Huku kwa Jacob asubuhi walikuwa kwenye Nyumba ya bwana Jacob na walikuwa wanapeana pongezi kwa kazi nzuri waliyoifanya, kutokana na pesa Jacob alizowapa wale vijana siku hiyo, yaani hawakuacha kumsifia Jacob maana kuna wengine kati yao walikuwa hata laki moja hawajawahi kuishika, sasa Jacob alivyo wapatia laki tano tano walimuona kama Mungu mtu, Jacob ili kuwafanya wazidi kumsaidia kazi zake zaidi na zaidi aliwaambia atawapa na makazi ya kulala maana walikuwa ni wazee wa kulala popote, baada ya hayo maneno hapo ndo walichanganyikiwa kabisa na kuona Jacob ndo anafaa kuwa Rais wa nchi kabisa (kweli kila mtu na mpambe wake)
Siku hiyo Jacob alifurahi kinoma maana alikuwa ni kama kapata kampani pale nyumbani yaani ilikuwa ni furaha kwa kwenda mbele.
Jacob alikuwa anajiachia kwa sababu alijua muda huo Mr Derick hawezi kuja kwa sababu atakuwa anaugulia maumivu ya kile kilicho mtokea.
Huku kwa Mr Derick mambo yalikuwa hayaendi vyema kabisa japo kuwa Mama Jacob alipona na kurudi kwenye hali yake ya kawaida ila ndo hivyo hali ya kiuchumi ilipungua kwa Jacob.
Baada ya lile duka la Mr Derick kuungua wale mabinti walio kuwa wanamsaidia Mama Jacob pale kuuza na wanapewa pesa ya kujikimu kila siku, tayari nao walipoteza ajira, wawili kati ya hao watatu waliingia kwenye biashara ya kujiuza, ila mmoja aliyebaki ilibidi aanze kuzunguka kutafuta kazi na alikuwa kachoka siyo poa na huyu siyo mwingine ni yule mdogo wake na shaifa aliye julikana kwa jina la Sharifa.
Yaani Sharifa maisha yalikuwa yamembadilikia na alikuwa kachakaa siyo poa, uzuri wake wa asili ulikuwa hauonekani tens na sijui ni kitu gani kilimpata mpaka kufikia kwenye hali ile.
Jacob akiwa na gari lake anakula mitaa, alifika maeneo fulani, ambapo baada ya kuangalia vizuri kuna mzee alimuona na alimkumbuka vizuri, hapo ilimbidi ashuke kwenda kusalimia.
"Babu shikamo" Jacob baada ya kushuka alisalimia
"Marhaba kijana karibu ukae bana tukuhudumie" yule babu alimkaribisha
"Babu mi sikai sana ila nilikuwa nakuja kukusalimia, sijui umenikumbuka lakini??" Jacob akiwa anajichekesha alimuuliza yule babu
"Uuuuuuu!! Hii sura siyo ngeni sana ila nimekusahau" Babu alivuta picha ni wapi alimuona Jacob ila hakukumbuka
"Babu mi kuna siku nilipita hapa, nikawa nakuuliza kwa mganga wa kienyeji na siku hiyo nilikuwa nahema sana umesahau" Jacob kumbe aliye kuwa anaongea naye ni yule babu muuza kahawa.
Ila wakati mazungumzo bado yanaendelea, kuna binti alifika pale akiwa kachakaa mno na alifika kwa babu pale akiwa anaomba kazi, ila Jacob alipo mwangalia vizuri alimkumbuka
"Heeee we Sharifa ni wewe ama naota??" Jacob alishangaa kumuona Sharifa akiwa kachakaa huku hatamaniki
Sharifa naye alishangaa kumuona Jacob, kutokana na yeye alivyo aliona aibu alishindwa hata kumwangalia Jacob usoni.
Jacob hata hakujali alimshika Sharifa mkono na kwenda naye kwenye gari bila hata kuongea chochote.
Baada ya kupanda kwenye gari Jacob alikanyaga mafuta mpaka nyumbani kwake huku akiwa hajazungumza kitu chochote na Sharifa.
"Jacob Mbona sikuelewi" Kwa uoga Sharifa aliongea baada ya kufika ndani
"Kabla ya yote ingia chumba kile pale nenda kaoge ujisafishe vizuri na nguo za kubadilisha zipo huko huko alafu baada ya hapo ndo uje tuzungumze"Jacob alimwelekeza Sharifa.
Sharifa naye hakuwa mbishi alienda kuoga vizuri na alianza kubadisha nguo, ila sharifa kitu alicho shanga zile nguo alizoambiwa zipo kwenye kabati abadilishe zilikuwa zinanukia manukato ambayo Dada yake shaifa alikuwa anatumia na Sharifa alikuwa hajawahi kuyaona manukato hayo popote zaidi ya kwa Dada yake.
Akiwa ni mwenye maswali mengi sharifa alitoka akiwa kapendeza angalau sasa alikuwa anaonekana ni mrembo miongoni mwa warembo japo bado alikuwa hajawa kama wa mwanzo.
"Jacob inamana Dada shaifa anaishi hapa??" Baada tu ya kukaa Sharifa hakutaka kusubiri aliamua kuuliza juu kwa juu
"Kwa nini umeuliza hivyo??"
"Uuu! Jacob bila shaka hizi nguo anayevaa ni Dada shaifa kwa sababu manukato ya hizi nguo ni ya dada shaifa" Sharifa alikuwa na uhakika asilimia 💯 kwamba zile nguo ni za shaifa.
Baada ya maswali mengi, Jacob ilibidi aanze kumsimulia Sharifa kila kitu kilivyo tokea mpaka mwisho na hilo lilimfanya Sharifa alie sana tena sana.
"Sharifa, kabla Dada yako hajafa aliniomba nikutafute popote ulipo nikulee vizuri, ila naomba nisamehe nimechelewa kukupata ila kwa vile upo hapa naahidi hutapata tena shida" Jacob alimtia matumaini Sharifa na kumnyamazisha.
Upande wa Mr Derick alikuwa anaaanda tena plani ya kumkabili Jacob maana kutokana na kuyumba kiuchumi kidogo, hapo alijua njia pekee ya kutamba mjini tena kwa mara ya pili ni kurudisha zile mali za bwana Jacob mikononi mwake tena, na Derick bado alikuwa hajajua ni nani aliye msababishia matatizo kiasi kile, ila kwa mbali alikuwa anamhisi Vicky, maana tangia waachane na Vicky walikuwa ni kama paka na panya, Derick alikuwa hamfikirii Jacob kwamba anaweza fanya tukio kama lile maana Yeye siku zote alikuwa anaamini kama Jacob ni mtu dhaifu daima.
Huku kwa Jacob pamoja na vijana wake walikuwa wanaliandaa pigo lingine kwa Mr Derick, maana Jacob katika peleleza yake aligundua bwana Derick bado hajakoma kumfuatilia.
Itaendelea..........
Usikose sehemu ya 51.

Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Write your comment